Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Abbas Ka‘bī, katika hafla ya uzinduzi wa kitabu Fiqhu al-Khabar kilichoandikwa na Hujjatul-Islam wal-Muslimīn Muhammad Mahdī Muhaqqiqī, iliyofanyika jioni ya Jumamosi makao ya Shirika la Habari la Hawza, alisema:
“Nawapongeza waandaaji wa hafla hii na hasa mwandishi wa kitabu hiki. Nina furaha kushiriki katika hafla hii yenye thamani, na ninatoa shukrani kutokana na juhudi za Hujjatul-Islam Muhaqqiqī kwa kuandika kitabu kuhusu fiqhu ya vyombo vya habari. Amechukua hatua muhimu kueleza misingi ya kisheria na kimaadili ya shughuli za vyombo vya habari.”
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum Iran, akielezea nafasi ya vyombo vya habari katika zama hizi, aliongeza kusema: “Leo chombo cha habari si tu kifaa cha kutoa taarifa, bali ni nyenzo ya kitamaduni na ya kistaarabu, ambacho katika mfumo wa Kiislamu kinapaswa kuendeshwa kwa mujibu wa fiqh, maadili na kanuni za dini. Fiqhi ya vyombo vya habari, kama vile fiqhi ya siasa au fiqh ya uchumi, inapaswa kuwa na kanuni na masharti yake maalum, na iwe ndiyo msingi wa utendaji wa vyombo vya habari kwa haki, uaminifu na kulinda manufaa ya umma.”
Wajibu wa vyombo vya habari katika mfumo wa Kiislamu
Ayatullah Ka‘bī alisisitiza: “Vyombo vya habari katika mfumo wa Kiislamu vina jukumu la kuhakikisha ukweli na uaminifu katika uenezaji wa taarifa na habari, na vina wajibu wa kuepuka kuchapisha uongo, uvumi au habari za kusingizia. Kuchapisha taarifa yoyote inayosababisha fitina, uharibifu au madhara kwa jamii ni haramu kisheria. Kinyume chake, utoaji wa taarifa sahihi, wazi na kwa wakati unaweza kuimarisha imani ya umma na kulinda maslahi ya kijamii.”
Umuhimu wa fiqh na maadili ya vyombo vya habari
Akiashiria umuhimu wa fiqh na maadili katika vyombo vya habari, alisema: “Kuheshimu maadili ya kidini, kitamaduni na kijamii ni jambo la lazima kwa vyombo vya habari. Chombo cha habari kinapaswa kuepuka vurugu, ufisadi na upotoshaji, na kifanye kazi ndani ya mipaka ya mafundisho ya Kiislamu. Hili si jukumu la viongozi wa vyombo vya habari pekee, bali pia ni wajibu wa waandishi wa habari, wahariri na wote wanaoshiriki katika kazi ya habari.”
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum Iran aliendelea kusema: “Miongoni mwa masuala muhimu katika fiqhu ya vyombo vya habari ni suala la ‘mlango wa habari’ (gatekeeping), yaani jukumu la wale wanaochagua na kuchapisha habari. Watu hawa wanapaswa kuwa waaminifu, waadilifu, na kutumia utaalamu wa wanazuoni wa dini; vilevile, wanapaswa kuheshimu haki za watu na faragha zao binafsi katika kuchapisha habari.”
Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi wa Dini (Majlis Khobregān-e Rahbarī) aliongeza kusema: “Kazi muhimu iliyofanywa na Hujjatul-Islam Muhaqqiqī katika kitabu hiki inaweza kuwa mwanzo wa kuunda mfumo kamili wa fiqh ya vyombo vya habari. Ni muhimu kwamba masuala haya yafundishwe na kufanyiwa tafiti hawza ili kuinua kiwango cha uelewa wa vyombo vya habari kwa misingi ya maarifa ya Kiislamu.”
Nafasi ya fiqh ya vyombo vya habari katika kupanga sera za habari
Ayatullah Ka‘bī aliendelea kusema: “Vyombo vya habari katika mfumo wa Kiislamu havipaswi kuwa tu vyombo vya kusambaza yaliyomo, bali vinapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa fiqh, maadili na kanuni za kisheria. Shughuli zote kuanzia utayarishaji hadi uchapishaji wa maudhui, zinapaswa kuchunguzwa mara kwa mara, kulinda haki za watu, kuheshimu faragha zao, na kuepuka kuchapisha mambo ya kuchochea, kuharibu au kupotosha, ni misingi muhimu ya fiqhi ya vyombo vya habari.”
Aliendelea kusema: “Vyombo vya habari vinapaswa kufanya kazi katika mfumo madhubuti katika eneo la utungaji sera, hasa katika uwanja wa mitandao ya kidijitali, kwa kufuata sheria na taratibu, ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza. Kuhakikisha usalama wa taarifa na kubadilishana data, kudhibiti maudhui yanayozalishwa, na kuelekeza hadhira kwenye maudhui yenye elimu na yanayojenga utamaduni ni miongoni mwa majukumu muhimu ya vyombo vya habari katika zama za kidijitali.”
Sera za vyombo vya habari vinavyotegemea fiqh zitengenezwe kwa umakini
Ayatullah Ka‘bī alisema: “Katika mazingira ya sasa ambapo akili bandia (AI) na teknolojia mpya vimeingia katika vyombo vya habari, ni lazima sera za vyombo vya habari ziandaliwe kwa uangalifu kwa mujibu wa fiqh. Vyombo vya habari vinapaswa kuepuka kuchapisha maudhui ya uchochezi, yenye usumbufu au yanayopingana na maslahi ya umma. Lengo kuu ni kuunda mfumo wa vyombo vya habari ambao ni wa kielimu na wa kujenga utamaduni, bila kuchochea chuki, vurugu au ufisadi.”
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum Iran, alihitimisha kwa kusema: “Kuzingatia misingi hii na kutengeneza sera zenye msingi wa kifiqh kwa vyombo vya habari, kunaweza kusaidia kujenga mazingira salama na yenye afya ya vyombo vya habari, na kutumia uwezo wa kitamaduni na kielimu wa vyombo vya habari kwa manufaa ya jamii ya Kiislamu.”
Ayatullah Ka‘bī aliendelea kwa kugusia suala la jihadi ya vyombo vya habari, na kwa kueleza kwamba jihadi si jambo la kijeshi pekee, na kwamba vyombo vya habari, kama vile vinavyoweza kuwa chanzo cha mashambulizi, vinaweza pia kuwa nyenzo ya jihadi, uelimishaji na uongofu, alisisitiza akisema:
“Leo hii sisi, katika kukabiliana na adui, tupo katika uwanja wa vyombo vya habari; kwa hiyo, kuzingatia vipengele vya kimaadili, mipaka na masharti ya kifiqhu katika uwanja huu ni jambo la lazima.”
Mjumbe wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi wa Dini (Majlis Khobregān-e Rahbarī), akibainisha haja ya kufafanua upya dhana ya jihadi katika zama hizi, aliendelea kusema: “Ikiwa tutalichukulia jihadi kuwa ni jambo la kijeshi pekee, basi tutakuwa tumeghafilika na mojawapo ya nyanja muhimu zaidi za maisha. Jihadi ya vyombo vya habari inapaswa kupanuliwa na kujumuisha zana zote za kisasa za mawasiliano ili kuimarisha uwezo wa kukabiliana na vita laini (vita vya kifikra na kitamaduni).”
Jihadi ya vyombo vya habari; wajibu wa kisharia
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qum, katika hitimisho la hotuba yake, alisema: “Kukabiliana na upotoshaji, kuzuia uundwaji wa maamuzi bandia na kuzuia kuenea kwa uvumi, kunahitaji hatua za haraka na elimu ya umma. Jihadi ya vyombo vya habari ni wajibu wa kisharia na kitaifa, na inapaswa kufuatiliwa kama kipaumbele cha kimkakati.”
Mwisho wa taarifa
Maoni yako